Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe Mosi Mei, 2017 amesema
Serikali ya Awamu ya tano imepanga kufanya nyongeza ya kawaida ya kila
mwaka katika mishahara yani Annual increment, ambayo ilikuwa imesimama
kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na promosheni.
Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo
katika Sherehe za siku ya Wafanyakazi duniani zilizofanyika katika
Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema uamuzi wa Serikali wa
kuanza kutoa promosheni unatokana na kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa
Wafanyakazi hewa zaidi ya wafanyakzi kumi 19,000 walibainika kuwa
wafanyakazi hewa.
”Yale mambo yote yaliyokuwa
pending ikiwa ni pamoja na promosheni kwa sababu tulishindwa, unaweza
kupromoti mfanyakazi hewa hayupo,kwa sababu tungetoa promosheni wakati
kuna wafanyakazi 19,000 hewa,maanake tungepromoti na 19,000 na siajabu
na watu waliowaandika mule ndio wangeletwa katika mapendkezo ya
promosheni” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewaonya
watumishi ambao wamekuwa wakidanganya umri wa kustaafu ili waendelee
kufanya kazi kwa muda mrefu na kuwa siku zao sasa zimekwisha.
Katika hatua nyingine Rais
Magufuli amepiga marufuku uhamisho wa Wafanyakazi bila kuwalipa stahili
zao kutokana na kuwepo na tabia ya kuwahamisha wafanyakazi bila
kuzingatia taratibu hasa za malipo ya uhamisho.
”Sasa niwaombe wafanyakazi
yeyote akihamishwa hakuna kuhama mpaka umelipwa pesa ya uhamisho,kuanzia
juu mpaka chini,yeyote atakaye kuhamisha mwambie nipe hela yangu ya
uhamisho ninapoenda akishindwa usihame kaa hapohapo ufanye kazi” Amesema Rais Magufuli.
Amesema viongozi wengine wamekuwa
wakiwahamisha wafanyakazi kwa maslahi binafsi au visasi kutokana na
maendeleo wanayowapata wafanyakazi.
Rais Mgufuli amewahakikishia
wafanyakazi kuwa Serikali ya awamu ya Tano itaendelea kuwajali na kuwa
karibu nao katika kutimiza dhana ya utatu ya ushirikiano kati ya
Serikali, Wafanyakazi na Waajiri kwa lengo la kuleta maendeleo.
Aidha, Rais Magufuli amewaeleza
wafanyakazi mipango mbalimbali anayofanywa na Serikali katika kuwaletea
maendeleo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya ,ujenzi wa Reli ya
kisasa, utoaji elimu bila malipo na uboreshaji wa miundombinu katika
kuwaletea maendeleo wananchi.
Sherehe za Mei Mosi zilizofanyika
katika mkoa wa Kilimanjaro pia zimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge
Mhe. Job Ndugai, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Wabunge na viongozi
mbalimbali wa Chama na Serikali ambapo kauli mbiu inasema,” Uchumi wa
Viwanda uzingatie kulinda Haki, Maslahi na Heshima ya Mfanyakazi”.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Moshi, Kilimanjaro
1 Mei, 2017
EmoticonEmoticon