Monday, 1 May 2017

MH. William Lukuvi amemtahadharisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amemtahadharisha Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, John Wanga, kwamba endapo atashindwa kusimamia vema agizo la urasimishaji makazi holela na uandaaji wa hati miliki kwa wananchi, atatumbuliwa.

Alitoa tahadhari hiyo juzi baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa   urasimishaji na uandaaji wa hati za ardhi ambako Halmashauri ya Ilemela imetekeleza kwa asilimia moja kwa kuandaa hati 834 huku viwanja  vingine 16,000  vikiwa vimepimwa bila kuandaliwa hati.

 Lukuvi  ambaye alionekana kukasirishwa na hali hiyo alisema kushindwa kuandaliwa    hati hizo  ndani ya Halmashauri ya Ilemela ambayo ina maofisa ardhi  na watathmini zaidi ya 40 kmeisababishia  hasara   Serikali.

Alisema kazi hiyo ingefanyika ilivyotarajiwa serikali ingepata  mapato ya  Sh bilioni 2.5 kwa mwaka lakini kilichopatikana  ni Sh bilioni 1.3 tu.

“Hakuna halmashauri nchini iliyo na watumishi  wengi wa idara ya ardhi kama Ilemela na Nyamagana mara zote nimekuwa nikifikiria kuwahamishia wilaya nyingine kama Geita kwa Mheshimiwa Rais, Dk. John  Magufuli ambako hakuna hata mmoja.

“Lakini  leo pamoja na wingi wenu mnaandaa hati 834 huku viwanja 16,000 mkishindwa kuvikamilisha kwa muda niliotoa.

“Sasa Mkurugenzi nakuambia kwamba Serikali imewavumilia  vya kutosha na sasa kama hautabadilika kwa muda ambao nimekuongezea kuanzia sasa hadi Juni 30, mwaka huu   tambua kwamba kitambi chako kitapata pancha.

“Wewe mwenyewe utajua namna ya kuiziba pancha hiyo, hatuwezi kuimba wimbo huo huo kila mwaka.

“Kuna viti vitu vidogo vidogo vya hapa halmashauri  mnavifinyia kazi lakini suala ambalo ni la muhimu    mnashindwa kukamilisha.

“Nilikuwa namuona mkurugenzi ni mjanja   lakini anachokifanya hapa ni kama kutwanga maji kwenye kinu kwa sababu kodi ya ardhi haikusanywi,” alisema.

 Waziri alisema Halmashauri za Ilemela na Nyamagana  zinatakiwa zikamilishe hatua hiyo  Juni 30, mwaka huu atakapoifunga rasmi na kutangaza ‘masterplan’ ya Jiji la Mwanza ifikapo Agosti.

Aliwataka wananchi kutambua kuwa baada ya kufungwa  urasimishaji makazi haitatokea    tena  fursa ya namna hiyo.

Alisema wananchi ambao hawatakuwa na hati ya eneo analoishi watahesabika kama wavamizi, hivyo watapoteza haki yao na maeneo hayo yatachukuliwa na Serikali kwa shughuli nyingine.

Lukuvi alisema Serikali kuu imetenga Sh bilioni 22 kwa ajili ya masterplan ya   Mwanza ambayo itaanza kutekelezwa Agosti mwaka huu,  kazi ambayo  itafanywa na wataalamu kutoka China. 


EmoticonEmoticon