Mshambuliaji machachari wa Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Yohana Nkomola, amegoma kujiunga na vilabu vya ndani ya Tanzania zikiwemo Simba na Yanga, na kuweka wazi kuwa mpango wake ni kucheza nje ya Tanzania bila kupitia vilabu hivyo vikubwa nchini, ili kukuza na kulinda kiwango chake.
Nkomola ambaye ni zao la Kituo cha Kuzalisha Vipaji cha Azam FC (Azam FC Academy), amefunguka wakati wa mahojiano na Azam News, na kuongeza kuwa hata mipango yake ya kucheza soka nje ya Tanzania ikikwama, hatakuwa tayari kujiunga na klabu yoyote nchini, isipokuwa ile itakayokidhi masharti yake.
Amesema timu kadhaa nchini zimekuwa vikimnyemelea zikiwemo Simba na Yanga lakini amezigomea huku akikanusha taarifa za kupata timu nchini Afrika Kusini pamoja na wachezaji wengine wa Serengeti Boys.
Kuhusu majaribio aliyokwenda kuyafanya katika klabu ya Etoile Du Sahel nchini Tunisia, Nkomola amesema majibu ni mazuri na anachosubiri ni makubaliano kati ya timu hiyo na wakala wake.
“Kuhusu majaribio yangu, nilishajibiwa kuwa nimefaulu, na timu ile imenipenda, hapa nilipo nasubiri kuitwa tu kwa ajili ya mkataba, sijui wamefikia hatua gani maana wanazungumza na wakala wangu,” alisema Nkomola.
EmoticonEmoticon