Thursday, 29 June 2017

Baada Donald Ngoma kuongeza mkataba wa kuichezea Yanga.

Baada Donald Ngoma kuongeza mkataba wa kuichezea Yanga, kocha George Lwandamina amesema kitu alichokifanya Ngoma ni cha kupongezwa

Baada ya mshambuliaji Donald Ngoma, kuongeza mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga, kocha mkuu wa timu hiyo George Lwandamina, amesema kitu alichokifanya Ngoma ni cha kupongezwa.


Lwandamina ameiambia Goal, anamuhitaji sana Ngoma kwenye kikosi chake cha msimu ujao hivyo kitendo cha kuongeza mkataba kimempa matumaini ya kufanya vizuri msimu ujao.

“Ni jambo zuri na wachezaji wengine wanatakiwa kuiga mfano wake Ngoma ni mchezaji anayestaili kuichezea Yanga kutokana na rekodi yake aliyoifanya akiwa na timu hiyo huko nyuma,”amesema Lwandamina.

Mzambia huyo amesema baada ya kushindwa kumtumia kwa muda mrefu msimu uliopita anaamini msimu ujao atakuwa na nafasi kubwa ya kutimiza majukumu yake uwanjani na kuwafurahisha mashabiki wao.

Amesema kubaki kwa Ngoma kwenye kikosi cha Yanga kutaongeza hofu hata kwa wapinzani wao, na kuendelea kuiogopa timu hiyo msimu ujao.

“Kuwa na Ngoma tunapata uhakika wa kuogopwa na wapinzani wetu kwani wamekuwa wakimuhofia sana hiyo ni faida kwetu ambayo tunapaswa kuitumia vyema kupata pointi tatu,”amesema.

Ngoma amesaini Yanga, mkataba wa miaka miwili, na kuzima uvumi ambao ulikuwa umeenea kuwa yupo mbioni kujiunga na wapinzani wao Simba ambao nao walikuwa wanamuhitaji.

Mzimbabwe huyo ameigarimu Yanga dola 420,000 kwa ajili ya mkataba huo utakaomuweka Jangwani hadi mwishoni mwa msimu wa 2019.


EmoticonEmoticon