Bofya hapa kwa habari za michezo zaidi.
Nahodha wa zamani wa klabu ya Everton, Leon Osman leo asubuhi amekutana na wachezaji wenye vipaji vya mchezo wa soka katika ziara fupi iliyofanyika uwanja wa Taifa Dar es Salaam, na iliandaliwa na Kampuni ya SportPesa ambao ni wadhamini wa klabu tatu nchini za Simba, Yanga na Singida United na kwa England ni Everton.
Osman ameongoza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu ya Everton, Robert Elstone,amefurahi kuona wachezaji wengi wenye vipaji vya hali ya juu tofauti na alivyofikiria.
“Ukweli sikutegemea kama nitaona wachezaji wenye uwezo mkubwa kama hawa ombi langu mimi ni moja kwa viongozi wa chama cha soka Tanzania TFF, pamoja na klabu zinazodhaminiwa na Sport Pesa, kuitumia vizuri kampuni hii kwani watanufaika nao sana ikiwemo kupata mafanikio ya ndani na nje ya uwanja,”amesema Osman
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, pia Ofisa Mtendaji Mkuu wa SportPesa Tanzania, Pavel Slavkov.
Kampuni ya Sport Pesa, imewasili nchini hivi karibuni na kujitolea kuzidhamini timu hizo tatu lakini pia imeandaa michuano maalumu ya Sport Pesa Super Cup, inayoshirikisha timu nane nne kutoka Tanzania na nyingine nne kutoka Kenya.
Mashindano hayo yamepangwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Juni 5 hadi 12 na mshindi atajinyakulia milioni 50, pamoja na kombe.
Kwa Tanzania timu ambazo zitashiriki ni Simba, Yanga, Singida United na Jang’ombe Boyz ya Zanzibar wakati kwa Kenya ni Gor Mahia, AFC Leopard, Tusker FC na Nakuru All Stars.
Osman aliichezea Everton katika Ligi Kuu England na michuano mingine tokea mwaka 2000 hadi 2016 alipotangaza kustaafu akiwa mmoja wa manahodha.
EmoticonEmoticon