SIRI kubwa imefichuka ya kuchezwa fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (FA) katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, kati ya Simba na Mbao FC.
Uamuzi wa fainali hiyo itakayopigwa Mei 28, mwaka huu kupelekwa Dodoma, ilikuja baada kuelezwa kwamba uwanja wa Taifa utafungwa kupisha matengenezo.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari kutoka Dodoma, kilisema kuwa siri kubwa ya fainali hiyo kuchezwa mkoani humo, kuwa ni kuhusiana na uchaguzi Mkuu wa TFF ambao utafanyika baadaye mwaka huu.
Chanzo hicho kilisema kuwa tayari kuna mipango ya chini kwa chini inadaiwa kufanywa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi, kumpigia kampeni Mwenyekiti wa Chama cha soka cha Dodoma, Mlamu Ng’ambi ambaye anamtaka kuwa makamu wake kwenye uchaguzi ujao wa TFF.
“Hii fainali ina mambo mengi lakini kwa taarifa yako amewaalika baadhi ya wajumbe wanaomuunga mkono wahudhurie fainali Dodoma ili wakajipange kuhusu uchaguzi,” kilisema chanzo hicho.
Aidha, chanzo hicho kilisema kuwa kumekuwa na mikakati mingi ya kiuchaguzi mwaka huu ndiyo maana hata ligi imekuwa ikiyumbishwa kwa sababu za uchaguzi wa TFF.
Mtoa habari huyo alikwenda mbali zaidi na kuliambia BINGWA kuwa wajumbe wote walioalikwa katika fainali hiyo watalipiwa usafiri wa ndani, posho ya kutosha na huduma nyingine muhimu wakapokuwa Dodoma.
Kwa mujibu wa kanuni, Simba ndio wenyeji wa mchezo huo kwa sababu ndio walitangulia kutinga fainali hizo kwa kuwafunga Azam bao 1-0 kwenye mchezo wa nusu fainali kabla ya Mbao walioichapa Yanga bao 1-0 kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali, katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
EmoticonEmoticon