Nilipokuwa natoa mada kuhusu miaka 50 ya Azimio la Arusha niliongelea pia suala la umakini wa viongozi katika kauli zao. Kwamba Kiongozi lazima ujue unatoa kauli gani wakati gani. Niliwaeleza wanachama na wageni wengjne katika mkutano wa ACT Wazalendo kuwa Amri ya kiholela aliyoitoa Rais John Magufuli kuzuia usafirishaji wa Mchanga wa Dhahabu imepelekea nchi yetu kupoteza USD 880m
Hivi sasa nchini kwetu kuna
sheria ya kutoza 20% ya thamani ya mauzo iwapo kampuni zinauziana hisa. Tozo
inayotozwa inaitwa Capital Gains Tax. Kodi hii mpya ilitungwa mwaka 2012 ili
kukabili wawekezaji waliokuwa wanauziana makampuni juu Kwa juu bila Tanzania kupata
lolote. Tanzania
imeshafaidika na kodi hiyo Kwa mauzo mbali mbali ambayo yamekwisha fanyika
kwenye sekta mbalimbali.
Wakati Rais anatoa AMRI kuhusu
Mchanga wa madini kusafirishwa kwenye nje ya nchi kulikuwa na mazungumzo
yanaendelea kati ya Kampuni ya Acacia mining ( yenye Assets zinazozalisha
nchini Tanzania tu kwa sasa
- Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara) na kampuni nyingine ya nchini Canada kuhusu
Acacia kununuliwa Kwa USD 4.4bn. Mara baada ya amri hiyo mazungumzo yalivunjika
na hivyo mauzo kutofanyika.
Iwapo Rais angechelewa kutoa
kauli yake Kwa wiki moja tu mazungumzo yale yangepelekea mkataba wa mauzo
kusainiwa na hivyo Serikali ingepata 20% ya thamani ya Mauzo Kama kodi ya
Ongezeko la Mtaji ( capital gains tax ). Hivyo kauli ya Rais imesababisha
hasara Kwa nchi yenye thamani ya USD 880m sawa sawa na shilingi 1.8
trilioni.
Tafiti zinaonyesha kuwa gharama
ya kujenga ' refinery ' ya kuchenjua dhahabu hapa nchini ni USD 800m. Hivyo
mapato ambayo yangepatikana kutokana na kodi ya mauzo ya Acacia yangewezesha
nchi kujenga refinery na kufikia lengo la Rais la kuwa na uchenjuaji wa mchanga
ule hapa hapa nchini. Rais angetulia angeweza kuua ndege wawili Kwa jiwe moja,
1) kiwanda cha kuchenjua kingejengwa nchini na 2) mchanga usingesafirishwa tena
kwenda China na Japan .
Hata hivyo Tanzania haina
mchanga wa kutosha wa kushibisha hiyo refinery Kwa mujibu wa teknolojia ya sasa
( soma maelezo yangu hapa chini Kwa Mhariri wa RaiaMwema). Hivyo Rais angeweza
kutumia mapato hayo Kwa matumizi mengine ya Maendeleo. Kwa mfano Bunge
lilitenga kama USD 430m hivi kujenga Reli ya
kisasa na tayari Serikali imeshaingia mkataba na kampuni kutoka Uturuki kujenga
Reli hiyo kipande cha Dar es salaam mpaka Morogoro. Lakini gharama ya kipande
hicho ni USD 1.2bn. Kwahiyo Rais angeweza kutumia mapato haya ya mauzo ya
Acacia kuongezea kwenye kipande hiki na hivyo kuepuka kukopa kuziba nakisi ya
USD 800m iliyopo Sasa na Bunge kwenye Bajeti ya 2017/18 lingetenga fedha za
kuanzia Morogoro kwenda Dodoma .
Kama Mipango ya Reli ipo sawa,
Rais angeweza kutumia fedha za capital gains tax kutoka Acacia kujenga vyuo vya
VETA kila Wilaya na kila Kambi ya JKT na chenji ingebaki. Tanzania
inahitaji tshs 750 bilioni kujenga vyuo vya VETA kila Halmashauri ya Wilaya,
Miji, Manispaa na Majiji nchini.
Rais angejifunza kujizuia kutoa
matamko barabarani angeisaidia Sana
nchi na kujisaidia yeye mwenyewe kutimiza ndoto zake kwa nchi anayoongoza. Mimi
binafsi naunga mkono kuwa ni lazima tuchenjue dhahabu hapa hapa nchini badala
ya kupeleka mchanga Japan na
China .
Lakini ni muhimu maamuzi hayo yawe na ushahidi wa kisayansi badala ya matamko
holela ambayo madhara yake Kwa nchi ni makubwa mno.
Arusha
26/3/2017
EmoticonEmoticon