SERIKALI imetoa vibali vya ajira mpya kwa nafasi 9,721, na
imeahidi kuendelea kuhakikisha utumishi wa umma unaendeshwa kwa kuzingatia
misingi ya utawala bora kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu.
Kati ya nafasi hizo, vibali 3,174 zimetolewa kwa Jeshi la
Polisi, Jeshi la Magereza nafasi 1,000, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji 8,523
nafasi 297 kwa Uhamiaji na nafasi 50 kwa ajili ya ajira za wataalamu wa afya
katika Hospitali ya Kisasa ya Mloganzila iliyopo jijini Dar es Salaam.
Aidha, kibali cha ajira kwa nafasi 4,129 za walimu wa
masomo ya Sayansi na Hisabati pamoja na nafasi 219 kwa ajira za mafundi sanifu
wa maabara za shule vilitolewa na taratibu za ajira kupitia Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angellah Kairuki
alipokuwa anawasilisha makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka wa Fedha wa
2017/2018 aliyeomba kuidhinishiwa jumla ya Sh 821,322,347,674 (Sh bilioni
831.3).
Kati ya fedha hizo, Sh 390,970,890,000 ni kwa ajili ya
miradi ya maendeleo wakati Sh 430, 351,457,674 ni kwa ajili ya matumizi ya
kawaida.
Aliongeza kuwa, Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira
katika utumishi wa umma, itaendelea kusimamia na kuendesha mchakato wa ajira
ili kuwezesha waajiri kupata watumishi wenye sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa
muundo wa utumishi husika.
Alisema wakati hao wakiombewa ajira, watumishi 19,708
wameondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma kutokana
na kustaafu, kuacha kazi, kufariki dunia, kufukuzwa kazi na kumalizika kwa
mikataba kwa lengo la kudhibiti watumishi hewa na mishahara batili.
Kuhusu uhakiki wa madai ya malimbikizo ya watumishi,
alisema madai 18,823 yenye thamani ya Sh bilioni 32.8 (32,859, 479,490.37)
yamehakikiwa na kuingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mshahara kwa
ajili ya malipo.
Aidha, madai ya malimbikizo ya mshahara ya watumishi
12,973 yenye jumla ya Sh bilioni 21.6 (21,615,565,432.71) yanaendelea
kuhakikiwa.
Akizungumzia bajeti ya mwaka huu, alisema imezingatia
vipaumbele na matakwa ya Serikali ya Awamu ya Tano yenye kusudio la kuimarisha
uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma ili kuondokana na matumizi mabaya
ya rasilimali, ukiukwaji wa maadili ya uongozi na urasimu katika utoaji wa
huduma kwa wananchi.
“Tunaamini utumishi wa umma uliotukuka ni chachu ya
maendeleo kwa taifa lolote duniani, hivyo nasi pia tumejipanga kikamilifu
kuhakikisha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
pamoja na taasisi zake inatoa mchango maridhawa katika kufikia malengo kama
taifa na kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” alisema
Kairuki.
Alisema ofisi yake inaunga mkono kwa dhati juhudi
zinazofanywa na Rais John Magufuli za kupiga vita rushwa, ubadhirifu wa mali za
umma na ufisadi lakini pia wanaunga mkono hatua stahiki zinazochukuliwa na
viongozi katika ngazi mbalimbali ili kurejesha nidhamu na utumishi wa umma na
kuboresha huduma kwa wananchi.
“Tumeanza kuona mafanikio, lakini bado tunayo kazi kubwa
ya kufanya mbele yetu,” alisema na kuwataka wabunge wenye mapenzi mema kwa nchi
kuunga mkono juhudi za serikali.
Akizungumzia Mpango wa Utekelezaji wa mambo muhimu kwa
mwaka 2017/18, alisema kwa upande wa Ofisi ya Rais, Ikulu pamoja na mengi
mengine imepanga kujenga kuendelea na ujenzi wa Ikulu mpya ya Chamwino,
kukarabati Ikulu ndogo za Mwanza, Shinyanga, Mbeya na Moshi.
Kuhusu Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za
Wanyonge Tanzania (MKURABITA), alisema Serikali inakamilisha uandaaji na utoaji
hati za hatimiliki za kimila 11,184 katika halmashauri 14 za Rufiji, Musoma,
Sikonge, Chamwino, Kiteto, Meru, Geita, Makete, Kahama, Njombe, Misenyi,
Sumbawanga, Misungwi na Magu.
Source: Habari Leo.
EmoticonEmoticon